Makala haya yanachanganua jinsi dhana za kifalsafa zinavyoakisiwa katika ushairi wa Kiswahili yakizingatia hasa tenzi zilizoandikwa kuhusu historia za dola za Kiafrika baada ya kupatikana kwa Uhuru. Tenzi nyingi za kundi hili zilitungwa Tanzania wakati wa ujamaa, ndiyo maana itikadi zinazoelezwa zaidi katika tenzi hizi zinahusiana na falsafa ya ujamaa. Uelekeo huu unaonyeshwa katika uchambuzi wa Utenzi wa Pambazuko la Afrika uliotungwa na Mohammed Seif Khatib na kuchapishwa mwaka 1982, ambao unaakisi falsafa ya ujamaa, itikadi za umoja wa Afrika (Panafricanism) na upingani wa ukoloni, ukigusana pia na imani ya Afrika kuwa chanzo cha mawazo mengi ya kifalsafa (Afrocentrism).
Kwa namna hii, inaonekana kwa uwazi kwamba utungaji wa tenzi ni njia muhimu sana ya kueleza falsafa ya kisiasa na ya kihistoria katika utamaduni wa Kiswahili. Njia hii inalingana na njia nyinginezo: mawazo hayohayo yanaelezwa vilevile katika vitabu vya kitaaluma (kwa mfano, vitabu vya Mwalimu Nyerere kuhusu ujamaa), katika riwaya, au katika ushairi wa aina nyingine (kama vile mashairi, ngonjera, n.k.). Tenzi nyingine za hili kundi la ‘tenzi za Uhuru’ zinaakisi vilevile falsafa za aina nyingine, ikiwemo falsafa ya kidini inayotokana na dini ya Uislamu au falsafa ya ‘utu’, ambayo ina mizizi mirefu sana katika tamaduni nyingi za Afrika.
Kwa kumaliza, makala yanasisitiza kwamba, tukipenda kufahamu ‘falsafa ya Kiafrika’ ni nini, ni lazima tutazame njia zilizoko na vyombo vilivyoko katika tamaduni za Kiafrika vya kuelezea dhana na thamani, bila ya kutarajia kwamba njia hizo na vyombo hivyo vitakuwa vilevile au vitafanana kimsingi na vyombo vya kawaida vya kuelezea falsafa katika tamaduni za Magharibi (yaani maandishi ya kitaaluma kuhusu falsafa). Ushairi ni njia mojawapo, tena muhimu sana, ya
kueleza mawazo ya kifalsafa katika utamaduni wa Kiswahili, lakini ziko na njia nyingine, kama vile maelezo ya taaluma mbalimbali na tanzu nyingi za fasihi na sanaa, ambazo inafaa zitambulikane na ichambuliwe katika fani ya falsafa.
Identifer | oai:union.ndltd.org:DRESDEN/oai:qucosa:de:qucosa:11478 |
Date | January 2010 |
Creators | Rettová, Alena |
Contributors | University of London, Universität Mainz |
Source Sets | Hochschulschriftenserver (HSSS) der SLUB Dresden |
Language | English |
Detected Language | Unknown |
Type | doc-type:article, info:eu-repo/semantics/article, doc-type:Text |
Source | Swahili Forum 17 (2010), S. 34-57 |
Rights | info:eu-repo/semantics/openAccess |
Relation | urn:nbn:de:bsz:15-qucosa-94151, qucosa:11598 |
Page generated in 0.0024 seconds