Kutokana na tofauti za mazingira, tabia ya nchi na hali ya hewa, binadamu wamekuwa na tamaduni zinazotofautiana na kufanana kwa viwango mbalimbali. Miongoni mwa masuala yanayotofautiana na kufanana ni majukumu yanayofanywa kwa kuzingatia misingi ya jinsi. Kutokana na umuhimu wa suala hilo, kumezaliwa taaluma ya jinsia inayohusu uhusiano uliopo baina ya wanaume na wanawake. Taaluma hiyo inaitwa ujinsia. Kwa miaka ya hivi karibuni msisitizo mkubwa kwa wanataaluma wengi, hasa wanaharakati wanaopigania haki na usawa wa wanawake dhidi ya ukandamizaji unaofanywa na wanaume, umekuwa ukidadisi mgawanyo wa majukumu kati ya wanawake na wanaume. Majukumu hayo yameenea karibu katika kila kona ya maisha ya binadamu toka katika siasa, uchumi na majukumu ya kijamii kwa ujumla. Imekuwa ikidaiwa kuwa katika uhusiano baina ya wanawake na wanaume, wanawake wamekuwa wakinyanyaswa na kukandamizwa. Kwa maneno mengine, uhusiano kati ya wanawake na wanaume haujajengwa katika misingi ya usawa kwa sababu wanaume wananufaika zaidi kuliko wanawake. Makala hii inachunguza namna mawazo hayo yanavyosawiriwa katika muziki wa taarab (mipasho) na nyimbo za ngoma ya Kibena iitwayo Mtuli. Tunachunguza namna majukumu ya mwanamke yanavyosawiriwa yakidokeza mgawanyo wa majukumu katika jamii zitumiazo sanaa hizo.
Identifer | oai:union.ndltd.org:DRESDEN/oai:qucosa.de:bsz:15-qucosa-107405 |
Date | 06 March 2013 |
Creators | Mnenuka, Angelus |
Contributors | University of Dar es Salaam, Taasisi ya taaluma za Kiswahili, Idara ya fasihi, mawasiliano na uchapishaji, Universität Leipzig, Institut für Afrikanistik |
Publisher | Universitätsbibliothek Leipzig |
Source Sets | Hochschulschriftenserver (HSSS) der SLUB Dresden |
Language | Swahili (individual language) |
Detected Language | Unknown |
Type | doc-type:article |
Format | application/pdf |
Source | Swahili Forum 19 (2012), S. 23-44 |
Page generated in 0.0022 seconds